Mitaa ya Zanzibar yaekewa anuwani za makaazi (Postcode)

Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeanza kutekeleza mradi wa uwekaji wa anuani za makaazi (postcode) kwa baadhi ya mitaa ya Zanzibar.Zoezi hilo limeanza kwa majaribio kwa baadhi ya mitaa ya Wilaya ya Magharibi kwa Unguja ikiwa ni pamoja na Shehia za Chukwani na Mombasa huku kwa upande wa Pemba ni kwa Shehia za Limbani na Selem katika Wilaya ya Wete. Kwa mujibu wa taarifa zinaeleza kuwa kiasi cha nyumba 4,324 katika shehia za Mombasa na Chukwani zimekusudiwa kuwekewa namba hizo.

Kwa upande wa Mombasa nyumba 2,439 na Chukwani 1,885. Uwekaji huo wa miundombinu ya postikodi ulizinduliwa rasmi na hadi kufikia Novemba 20 mwaka 2014, kwa shehia ya mombasa nyumba 2,177 kati ya 2,439 sawa na aslimia 89 tayari zimeshawekewa alama za postcode. Kwa shehia ya Chukwani nyumba 1,337 kati ya 1,885, sawa na asilimia 71 tayari zimeshawekewa alama za ‘postcode’.