Kaskazini Pemba: Mkoa uliotandikwa mtandao mpya wa barabara

Katika mwaka 2014 kama kuna Mkoa ambao unaweza kujivunia mafanikiomakubwa kwenye ujenzi wa Miundombinu ya barabara ni mkoa wa Kaskazini Pemba. Kwa hakika Mkoa huo, ujenzi wa barabara tano zilizozinduliwa utabakia kuwa ni historia ambayo itachukua muda mrefu kusahaukilika. Mapema mwaka jana , Rais wa awamu ya saba Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein alifungua barabara tano katika Mkoa wa Kaskazini Pemba. Barabara hizo zilijengwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Watu wa Marekani kupitia mfuko wa changamoto za Millenia (MCAT). Barabara hizo zilizofunguliwa na Mhe. Rais ni pamoja na Kipangani-Kangani, Chwale-Likoni, Mzambarautakao-Pandani-Finya, Mzambarau Kariminya -Finya –Mapofu na Bahanasa-Daya –Mtambwe.

Baada ya kuzifungua rasmi barabara hizo Dkt. Shein alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa mikoa yote ya Pemba ambapo aliwanasihi kuzitunza barabara hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu zaidi kwani pesa zilizotumika hapo ni pamoja na kodi za wananchi wenyewe. Hata hivyo Dkt. Shein aliwataka wananchi hususani waendesha magari kuendesha polepole na wazingatie alama za barabarani ili kuepusha ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikisababisha vifo na ulemavu. Katika hafla hiyo, aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Mhe. Rashid Seif Suleiman, aliishukuru Serikali ya watu wa Marekani kwa kusaidia ujenzi wa barabara hizo pamoja na misaada mingine ya kijamii kwa wananchi wa Zanzibar. Hata hivyo, Waziri huyo wa zamani alisema kujengwa kwa barabara hizo kutazidi kuwapa fursa wananchi wa maeneo ambayo umepita mradi huu na maeneo ya jirani kuweza kufanya shughui zao za kiuchumi na kijamii kwa ufanisi zaidi kutokana na kuimarika huduma za usafiri. Aidha aliiomba Serikali ya watu wa Marekani kupitia mfuko wake wa changamoto za millennia kuzidi kuisaidia Zanzibar ili iweze kwenda sambasamba na ulimwengu wa sasa. Akitoa maelezo ya kitaalamu Katibu

Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Dkt. Juma Malik Akil alisema ujenzi wa barabara hizo ni moja ya utekelezaji wa sera ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuwaondolea tatizo la usafiri kwa kuwajengea miundombinu ya kisasa ya usafiri. Pia ujenzi huo wa barabara ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ‘vision’ 2020, mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar MKUZA II pamoja na sera ya usafirishaji Zanzibar (National Transport Policy).

Dkt. Akil alifahamisha kuwa barabara hizo zimejengwa kwa mchanganyiko wa lami ya baridi na kokoto (surface dressing) ambayo ni madhubuti na yenye kudumu kwa muda mrefu. Alisema barabara hizo zimejengwa kwa kuzingatia utaalamu kwa kuekewa ‘road reserve’ kwa maendeleo ya baadae ambazo ni mita 12.5 kila upande.

Kwa upande wake aliekua Kaimu Balozi waMarekani nchini Tanzania, Mhe. Virginia Blaser alisema mradi huo utawapa wakaazi wa Kaskazini Pemba uwezo wa kufikia kwa urahisi huduma mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na shule, vituo vya afya na shughuli nyengine kama masoko. Barabara hizi zilijengwa chini ya usimamizi wa shirika la millennium challenge Account- Tanzania (MCAT-Tanzania) na kufadhiliwa na watu wa Marekani.

Aidha kampuni ya LEA Associates South Asia Pvt Ltd kutoka India Iliyofanya kazi ya usimamizi wa kihandisi kwa niaba ya MCAT ambapo mradi huu uligharimu shilingi za Kitanzania 38,247,180.00 kati ya hizo serikali ya Tanzania imechangia shilingi 21,773,055.00.