DK.Shein amekutana na uongozi wa Wizara ya Ujenzi , Mawasiliano na Usafirishaji
03 Sep 2019

DK.Shein amekutana na uongozi wa Wizara ya Ujenzi , Mawasiliano na Usafirishaji

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji katika mkutano wa utekelezaji wa  mpango kazi wa Mwaka wa Fedha kwa kipindi cha Julai  2018-Juni 2019 na mpango kazi wa mwaka 2019-2020 uliofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar,03/09/2019.

Baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Usafirishaji wakiwa katika mkutano wa utekelezaji wa  mpango kazi wa Mwaka wa Fedha kwa kipindi cha Julai  2018-Juni 2019 na mpango kazi wa mwaka 2019-2020 uliofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar,chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuna umuhimu kwa Wizara na taasisi za Serikali kushirikiana ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wakati.

Dk. Shein amesema hayo Ikulu mjini hapa, wakati akipokea taarifa za Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa mwaka 2018/2019.

Alisema kuna baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo imeshindwa kutekelezwa kwa wakati, kutokana na ukosefu mashirikiano, baada ya taasisi kuwa na mitizamo inayokinzana katika suala la uwekaji wa miundombinu.

Alieleza kuwa kabla ya mradi wowote wa maendeleo kuanza kutekelezwa, ni muhimu kwa taasisi zenye miundombinu inayoingiliana kukaaa pamoja na kuangalia namna miundombinu hiyo itakavyowekwa, ili kuepuka gharama na uharibifu usio wa lazima.

Alisema kuna baadhi ya barabara zilizokatwa kwa ajili ya kupitisha miundombinu bila ya wenye mamlaka kuarifiwa, hivyo alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ustaarabu wa kufanyakazi kwa pamoja ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza.

Dk. Shein alitowa ufafanuzi huo baada ya Uongozi wa Wizara hiyo kuelezea changamoto kubwa ya uharibifu wa barabara unaotokana na baadhi ya taasisi kupitisha miundombinu, ikiwemo ya maji na taa.

Aidha, Dk. Shein alisema serikali itaangalia uwezekano wa kuijenga barabara ya Chake-Wete kwa nguvu za serikali, kwa kuzingatia tayari imejenga uwezo wa kiutendaji baada ya kununua vifaa mbali mbali vya ujenzi wa barabara.

Alisema hayo baada ya taarifa ya tathmin za awali zilizotolewa na Uongozi wa Wizara hiyo kuonyesha gharama kubwa za ujenzi na malipo ya fidia ya barabara hiyo kupitia mkandarasi.

Aliwataka mafundi na Mainjinia wa Wizara hiyo kuwa na uataratibu wa kukaa pamoja na kufanya tathmin ya gharama za ujenzi, kabla ya mradi wowote kuanza kutekelezwa, ili kuepuka na viwango vikubwa vya gharama vinavyotozwa na wakandarasi.

Aidha aliwataka viongozi wa Wizara hiyo kukutana na Viongozi wenzao (Wizara ya Mawasiliano) Tanzania Bara ili kuona mifumo ya kiusalama katika Viwanja vya ndege inafanyakazi kwa maslahi ya pande mbili za Muungano.

Dk. Shein alikumbusha umuhimu wa Bodi za taasisi na mashirika ya Serikali kutekeleza majukumu yao na kufanya maamuzi kisheria, huku akisisitiza haja ya taarifa zao kuwasilisha kwa Waziri anaehusika.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliutaka Uongozi wa Wizara hiuyo kuzingatia umuhimu wa matumizi sahihi ya mchanga kwa ajili ya miradi yake ya ujenzi wa barabara, kwa msingi kuwa rasilimali hiyo iliyobaki ni kidogo.

Alisisitiza uamuzi wa Serikali wa kutokuagiza rasilimali hiyo nje ya nchi, kwa vile hatua hiyo haina maslahi na Taifa.

Alisema Serikali itaendelea na udhibiti wa rasilimali zake, ikiwemo mchanga, kifusi na mawe, ili kuhakikisha kunakuwepo matumizi mazuri,  baada ya siku za hivi karibuni kubainika baadhi ya watu wakisaga vifusi kwa ajili ya matofali.

Alisema hivi sasa kumebaki maeneo sita pekee yenye mchanga katika ardhi ya kilimo, hivyo kuna hatari ya kuathiri upatikanaji wa chakula, endapo rasilimali hiyo itatumika kwa shughuli za ujenzi.

Aidha, akawataka viongozi wa Wizara hiyo kukaa pamoja na wadau wa usalama barabarani, ikiwemo Polisi, UUB na Manispaa kwa ajili ya kuangalia mahitaji ya uwekaji wa taa za kuongoza gari barabarani.

Alisema katika maeneo mbali mbali ya miji yenye makutano ya barabara Unguja na Pemba, kunahitajika kuwekwa taa za kuongoza magari pamoja na njia ya wenda kwa miguu (zebra cross), ili kupunguza uwezekano wa kutokea ajali za mara kwa mra, ikizingatiwa baadhi ya madereva na waendao kwa miguu hawafahamu sheria za usalama barabarani.

Alisema miji imekuwa na gari zimeongezeka, hivyo ni lazima kuwepo taa za kuongoza gari katika maeneo yanayoonekana hatarishi ili kuepuka ajali, sambamba na kutaka kuwepo matumizi mazuri ya barabara kuanzia hatua za upatikanaji wa leseni.

Aidha, Dk. Shein aliukumbusha uongozi huo kuwa Serikali imetumia gharama kubwa kufanikisha uwekaji wa Mkonga wa Taifa, hivyo akasisitiza matumizi yake kuwa ni ya umma.

Akinasibisha na kauli yake, alizitaka taasisi zote za Serikali zenye kutoa huduma nchini kukaa pamoja na taasisi nyingine na kutafuta ufumbuzi pale zinapojitokeza changamoto, ikiwemo madeni, badala ya taasisi moja kuikatia huduma taasisi nyingine.

Vile vile, Dk. Shein alisema ili Wizara iweze kupata maendeleo endelevu ni jukumu la kila Idara na taasisi za Serikali kufanya utafiti utakaoleta matokeo ya haraka na kuondokana na dhana kuwa Idara ya Mipango, Sera na Utafiti ndio pekee yenye jukumu hilo.

Alisema hii ni mara ya kwanza katika hsitoria ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kupata fedha zaidi ya shilingi Bilioni 131.6 , akibainisha hatua hiyo inatokana na dhamira ya Serikali ya kuimarisha Wizara hiyo yenye umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa,

Alitowa pongezi kwa Uongozi wa Wizara hiyo na kubainisha kuridhishwa kwake kutokana na utekelezaji wa majukumu, sambamba na uwasilishaji mzuri wa taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi.

Mapema, Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Sira Ubwa Mamboya alisema katika kipindi hicho Wizara imepata mafanikio makubwa, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa kilomita 28 za barabara mbali mbali Unguja na Pemba kwa kiwango cha lami, ikihusisha kilomita 16 za barabara ya Ole – Kengeja, kilomita tatu za barabara ya Wawi – Mabaoni na kilomita tatu za barabara ya Mkanyageni – Kangani.

Alisema Wizara hiyo imefanikiwa kuweka Taa za kuongezea magari katika maeneo ya matano ya makutano ya barabara Unguja na Pemba, ambayo ni kwa Biziredi, Mlandege na Mtoni Jeshini (kwa Unguja) pamoja na Mtemani Wete na Chake chake PBZ kisiwani Pemba.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho Wizara imezifanyia matengenezo barabara mbali mbali kwa kuziwekea kifusi, kuziba mashimo pamoja na kuzifanyia usafi.

Aidha, alisema Wizara inaendelea na ujenzi wa Barabara ya Bububu – Mahonda – Mkokotoni yenye urefu wa kilomita 31, wakati ambapo kilomita 28.8 za barabara hiyo zikiwa tayari zimewekewa kifusi tabaka la mwisho, pamoja na kuweka lami ya maji kilomita 14 katika upande mmoja wa barabara.

Dk. Sira alisema katika kipindi hicho Wizara imekamilisha ujenzi wa mtaro wenye urefu wa kilomita 1.5 katika barabara ya Kiembesamaki, huku ikiendelea kumalizia hatua za mwisho za ujenzi wa daraja katika eneo la Kibonde Mzungu, mradi unaohusisha uwekaji taa, ujenzi wa kingo za pembeni (guardrail) pamoja na uwekaji wa lami ya mwisho.

Akigusia azma ya Serikali katika kuimarisha ujenzi wa miundo mbinu, Dk. Sira alisema Wizara imefanikiwa kununua vifaa mbali mbali vya ujenzi, ikiwemo vifaa 17 vya zana nzito, mitambo ya Lami, gari la kutandazia lami pamoja na gari la lami ya maji ambavyo tayari vimewasili nchini.

Alibainisha kuwa aina 13 ya vifaa vilivyosalia viko njiani kuja nchini.

Aidha, alisema Wizara imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Meli mpya ya Mafuta (MT Ukombozi 11), ambayo tayari imewasili nchini tangu Agosti 7, mwaka huu.

Dk. Sira alisema Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imefanikiwa kuimarisha huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) kwa kuimarisha Ulinzi na usalama , ufungaji wa mkanda wa mizigo, ununuzi wa mashine tano mpya za ukaguzi, kuimarisha Ukumbi wa Marais pamoja na kuendelea na ufungaji wa Vipoza hewa.

Alisema kwa upande wa Pemba, Wizara imefanikiwa kukamilisha upembuzi yakinifu wa Uwanja wa Ndege Pemba, unaoonyesha namna uwanja huo utakavyokuwa baada ya ujenzi na kubainisha kuwa hatua inayoendelea hivi sasa ni ya utafutaji wa fedha ili ujenzi huo uweze kuanza.

Katika hatua nyengine Waziri huyo alisema Wizara imefanikiwa kununua vifaa mbali mbali vya kufanyia kazi Bandarini, ili kuongeza ufanisi katika uhudumiaji wa mizigo.

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na vile vya kubebeba mizigo (Reachestaker moja, Mobile crean kubwa ya tani 55 pamoja an Folklift moja, Boti ya Rubani moja na Tishali la kuhudumia vyombo vya abiria katika Bandari ya Malindi.

Alibainisha kuwa malipo ya awali kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo tayari umefanyika na kazi ya matengenezo ya vifaa vilivyopo inaendelea.

Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe, alisema changamoto kubwa inayoikabili Wizara hiyo ni baadhi ya taasisi kukata barabara kwa ajili ya kupitisha hduma za kijamii, hivyo kuleta uharibifu mkubwaa wa barabara hizo.

Alisema kumekuwepo ukataji ovyo wa barabara kwa ajili ya kupitisha huduma za maji pamoja na umeme unaofanywa na taasisi bila kuzingatia gharama za utengenezaji wa barabara hizo.

“Kuna baadhi ya wakati taasisi mbili kwa nyakati tofauti hukata barabara kila mmoja na kupitisha miundombinu, jambo ambalo kama kungekuwepo ushirikiano kwa taasisi kukaa pamoja kabla ya ujenzi na kupitisha miundombinu yao katika eneo moja, kusingekuwa na uharibifu huu wa barabara”, alisema.

Wakati huo huo; Rais Dkt Shein alikutana na Uongozi wa Wizara ya Nchi (OR) na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kusisitiza haja ya Idara na taasisi za Wizara hiyo kufanya utafiti ili kupata mafanikio katika malengo yake.

Alisema ni muhimu kwa viongozi wa Idara kufanya tafiti mbali mbali, akibainisha hatua hiyo itawezesha kupata maendeleo endelevu.

Aidha, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kujenga mashirikiano na wafanyakazi wake, ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazokwamisha utendaji bora wa kazi.

Dk. Shein aliipongeza uongozi wa Wizara hiyo kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake, pamoja na kuwasilisha vyema taarifa za utekelezaji wa mpango kazi kwa mwaka 2018/2019. 

Nae, akiwasilisha taarifa ya mpango kazi kwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Waziri wa Wizara hiyo Issa Haji Ussi ‘Gavu’ alisema katika kipindi hicho Ofisi ya Rais iliendelea na ujenzi wa Ikulu ndogo Micheweni, ambapo hivi sasa imefikia hatua ya kuridhisha .

Alieleza kuwa ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Chake chake Pemba unaendelea vizuri,  ukitarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Aidha,  alisema Serikali imekuwa na mahusiano mema na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kupitia Makongamano ya kila mwaka.

 

Mawasiliano

Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
P.O.Box 266
ZANZIBAR
TANZANIA

190 FUMBA ROAD
POSTCODE: 71201
ZANZIBAR, TANZANIA

email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.