Mafunzo kwa watendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar
06 Apr 2021

Mafunzo kwa watendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar

 
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil Bakari akisoma taarifa rasmin kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Rahma Kassim Ali ambapo pia alifungua mafunzo hayo.
 ZAIDI ya wafanyakazi 70 wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar, wamepatiwa mafunzo ya awali ya ulinzi na usalama yakiwa na lengo la kuhakikisha kwamba abiria na mizigo inayosafiri au kuingia nchini inakaguliwa kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika zinazosimamia usafiri wa anga ulimwenguni.
 
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Amour Hamil Bakari, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo, wasiridhike na mafunzo bali waendelee kujifunza zaidi Ili kuwa na ufanisi.
 
Alisema, Serikali ya awamu ya nane imechukua juhudi kubwa katika kuimarisha huduma za usafiri wa anga kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi na kuwaondolea usumbufu abiria pamoja na wananchi wa Unguja na Pemba.
 
Alisema Wizara kupitia sekta ya anga inaendelea na usimamizi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria (terminal III) na mpango wa kuimarisha Uwanja wa ndege wa Pemba na Kigunda Ili kusaidia sekta mbalimbali za kiuchumi zikiwemo Biashara, utalii na kilimo kusaidia kukuza uchumi na kupinguza umasikini nchini.
 
Aidha, Alisema Wizara itaendelea kusimamia na kuhakikisha wafanyakazi watakaofanyakazi katika maeneo ya viwanja vya ndege Zanzibar wanapatiwa taaluma ya kutosha ambayo itaenda sambamba na hali halisi ya ushindani na viwanja vyengine katika ukanda huu wa Africa Mashariki.
 
Sambamba na hayo, aliupongeza uongozi wa Mamlaka ya viwanja vya ndege kwa kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto ambazo zimekiwezesha kiwanja kuwa na huduma zote muhimu zinazohitajika katika viwanja.
 
"Wizara itaendea kutoa ushirikiano  kwa uongozi wa Mamlaka ili kukamilisha mipango bora ya maendeleo ya kukuzaa sekta ya anga iliyowekwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar" alisema.
 
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Zanzibar, Hamdan Omar Makame, Alisema matarajio yao Baada wafanyakazi kupatiwa mafunzo hayo, wataendelea kufanya kazi zao kwa mujibu wa mafunzo waliyopatiwa.
 
Hivyo, aliwataka kuwa makini katika mafunzo hayo Ili lengo lifikiwe na kuweza kuondosha changamoto zitakazoweza kujitokeza.
 
Nae, Mkuu wa Chuo cha usafiri wa anga Tanzania, Aristid Kanje, alisema kuwa katika kuboresha mafunzo hayo, Chuo kimeona ni vyema kuengeza mafunzo Ili kuona ufanisi wa kazi unapatikana.
 
Alisema, wafanyakazi hao ndio nguzo ya msingi ya kuhakikisha sekta ya usafiri wa anga inakuwa salama, ambapo wameengeza namna ya kidhibiti madawa ya kulevya, madini na nyara za serikali.
"Tumeona kwamba wafanyakazi wetu wengi hawatambui namna ya kuvitambua kwa hivyo tumeviengeza kama masomo haya Ili kuboresha".
 
Hata hivyo, alisema katika masomo waliengeza pia namna ya kujua mienendo ya watu kwenye viwanja vya ndege ambapo watu watakaotumia viwanja hivyo kwa malengo tofauti waweze kuwatambua.

Mawasiliano

Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
P.O.Box 266
ZANZIBAR
TANZANIA

190 FUMBA ROAD
POSTCODE: 71201
ZANZIBAR, TANZANIA

email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.